مقالات

Ali Mohamed Al-Shurafaa Al-Hammadi anaandika: Uislamu ni Wito wa Amani, Mageuzi, na Uadilifu Muhtasari

Katika tahariri ya toleo la 11 la jarida la “Al-Arab” (Toleo la Kimataifa) la mwezi Juni 2026, Mwanafikra mkubwa wa Kiarabu Ali Mohamed Al-Shurafaa Al-Hammadi anazungumzia misingi mikuu ya Uislamu inayounda kiini cha dini sahihi, anasema kuwa Uislamu ni mfumo kamili wa maisha wa kiakili na kiroho unaofanya usawa kati ya maada na roho. Anaeleza kuwa Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume wake Muhammad kama rehema kwa walimwengu wote, na si kama mtume wa vita na udhalimu, bali alimtuma kama mwalimu anayewaongoza watu na kuwatoa kutoka kwenye giza kwenda kwenye nuru.
Al-Shurafaa Al-Hammadi anaendelea na mazungumzo yake kwa kuibua kadhia nyingine muhimu sana na kuifanyia marekebisho sahihi, nayo ni suala la nani anayemiliki hukumu ya ibada Akhera. Anasema: “Hukumu ni ya Mwenyezi Mungu pekee, Yeye ndiye Mjuzi wa yaliyofichikana, Yeye ndiye anayeshika sheria na kupanga mambo, na watu wanapaswa kusoma Kitabu chake; kwani hakuna yeyote mwenye mamlaka juu ya sheria Yake, na hakuna mabadiliko katika hukumu Yake.”
Kisha Al-Shurafaaa nahitimisha kwa kusisitiza wito wa Uislamu, akisema: “Uislamu haulinganii vurugu au kisasi, bali mageuzi na uadilifu, na rejea yake ni Qur’ani Tukufu ambayo inachukuliwa kuwa ni nuru yenye kuongoza na rejea kuu. Atakayeifuata amefanikiwa, na atakayeitupa amepotea. Uislamu uleule aliokuja nao Muhammad ndio uleule aliulingania Nuhu, Ibrahimu, Musa, Issa na mitume wengine wote a.s, hautofautiani isipokuwa katika umbo tu, lakini maudhui yake ni kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee na kushikamana na elimu na njia ya haki.”

Maelezo Kamili
Sio Ibada za Kidhahir tu
Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema katika maelezo ya toleo la 11 kuwa: “Uislamu sio tu dini inayotekelezwa katika ibada za kidhahiri, bali ni mfumo kamili wa maisha unaosimama juu ya kuwalingania watu kwenye amani, uadilifu, rehema na matendo mema. Kiini chake ni kumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja asiye na mshirika, kukataa dhuluma na uadui, na kushikamana na maadili ya heri na haki. Uislamu haufundishi chuki, bali hujenga ndani ya mwanadamu tabia ya rehema na kumwongoza kuishi kwa amani na wengine, huku ukikuza thamani ya ihsani kama msingi wa mahusiano ya kibinadamu. Ni wito wa dhati wa maisha mema, usiojengwa juu ya matambiko matupu, bali juu ya matendo mema, fikra safi na imani thabiti.”

Uislamu ni Mfumo wa Kiakili
Al-Shurafaa Al-Hammadi anaendelea na mazungumzo yake akisema: “Katika zama ambazo watu wanatafakari upya dhana na maadili yao, na kuanza kutumia akili zao kujielewa wenyewe na ulimwengu, Uislamu unajitokeza kama mfumo wa kiakili na kiroho unaofanya usawa kati ya maada na roho. Unashawishi mwanzo mpya ambapo mwanadamu anaishi kwa utulivu wa moyo, hata kama changamoto zitakuwa kali kiasi gani karibu naye. Yeyote anayeshika njia ya imani anapata faraja na amani moyoni mwake, lakini yule anayechagua uharibifu na kujitenga na njia ya Mwenyezi Mungu, anajiletea mwenyewe dhiki na tabu. Mwenyezi Mungu amefanya rehema, uadilifu na amani kuwa maadili ya asili yasiyobadilika, na hairuhusiwi kwa yeyote kuyapotosha au kuyatumia vibaya.”

Mtume wa Rehema, Si wa Ubabe
Kuhusu ujumbe wa Mtume, Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema: “Mwenyezi Mungu alimtuma Mtume wake Muhammad kama rehema kwa walimwengu wote, na si kama mtume wa vita na ubabe, bali alimtuma kama mwalimu anayewaongoza watu na kuwatoa kutoka kwenye giza kwenda kwenye nuru. Alikuwa akiwafundisha kwa kutumia Qur’ani, na hakuwa anamiliki elimu ya ghaibu wala uombezi (shifaa), bali alikuwa ni mja anayefunuliwa wahyi, aliyeamriwa kufikisha ujumbe na si kuwatawala watu wala kutawala hatima zao. Kama vile ujumbe ulivyosimama juu ya huruma, vivyo hivyo unalenga umoja wa wanadamu; kwani watu wote asili yao ni moja, na hakuna mbora kati yao isipokuwa kwa ucha Mungu na matendo mema. Kwa hiyo, kiini cha dini ya haki ni kimoja katika jumbe zote: kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee, kueneza heri, na kukataa ushirikina na uharibifu.”

 

Uislamu Hautoi Hati za Msamaha
Kuhusu nani anayemiliki hukumu na utungaji wa sheria, Al-ShurafaaAl-Hammadi anasema: “Hukumu ni ya Mwenyezi Mungu pekee, Yeye ndiye Mjuzi wa yaliyofichikana, Yeye ndiye anayeshika sheria na kupanga mambo, watu wanapaswa kusoma Kitabu chake, kuzitumia akili zao kuelewa aya zake, na kuongozwa na amri zake. Hakuna yeyote mwenye mamlaka juu ya sheria Yake, na hakuna mabadiliko katika hukumu Yake, hata uombezi haumilikiwi na mtume wala walii yeyote isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na yeyote anayedhani kuwa kuna asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayemiliki uombezi, basi amepotea. Uislamu hautoi hati za msamaha wa madambi kwa mtu yeyote, bali unaunganisha wokovu na imani pamoja na matendo mema, na si kwa kujisifu na ukoo au kuwaomba viumbe.”

Uislamu unalingania Kwenye Mageuzi na Uadilifu
Kuhusu wito wa Uislamu, mwandishi Ali Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema: “Wakati wa migogoro, Uislamu haulinganii kwenye vurugu au kisasi, bali kwenye mageuzi na uadilifu. Amani huanzia ndani ya nafsi kisha huonekana kwenye jamii, haipatikani kwa vurugu, bali kwa elimu, subira na neno zuri. Hata jihadi ya kweli sio kumwaga damu, bali ni kuisafisha nafsi, kupambana na matamanio, na kuikabili batili kwa hekima na mawaidha mema. Uislamu hauchochei vita, bali unaimarisha misingi ya amani; Hauwashi moto wa chuki, bali unauzima kwa rehema na uadilifu.”

Kuifuata Qur’ani ni Wokovu, na Kuiacha ni Dhiki
Kuhusu Qur’ani Tukufu, Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema: “Qur’ani Tukufu ni nuru yenye kuongoza na rejea kuu, ndani yake mna ufafanuzi wa kila kitu. Atakayeifuata amefanikiwa, na atakayeitupa amepotea. Muislamu wa kweli ni yule anayeifanya Qur’ani kuwa rafiki yake, na anayejitenga na dhuluma na uonevu, na anakuwa mfano wa amani na ucha Mungu katika zama za fitina. Uhusiano kati ya mwanamume na mwanamke katika Uislamu unajengwa juu ya mapenzi na rehema, si juu ya utawala au unyonyaji, bali juu ya ushirikiano na kusaidiana. Hakuna dhuluma katika dini ya Mwenyezi Mungu, bali kuna uadilifu unaoenda sambamba na heshima ya mwanadamu.”

Dini Mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu
Kuhusu dini ya haki iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu, Ali Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema: “Uislamu uleule aliokuja nao Muhammad ndio uleule aliokuja nao Nuhu, Ibrahimu, Musa, Issa na mitume wengine wote. Hautofautiani isipokuwa katika umbo tu, lakini maudhui yake ni kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee na kushikamana na elimu na njia ya haki. Mwenyezi Mungu amekamilisha dini hii, na ametimiza neema Yake, na akaishusha Qur’ani kuwa mwisho wa vitabu vyote; Kwa hiyo hakuna haja ya dini mpya, na hairuhusiwi kubadilisha amri za Mwenyezi Mungu au kuzikwepa. Mtume Muhammad hakuwa mungu wa kuabudiwa, wala bwana wa kutukuzwa, bali alikuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu, aliyekufa kama wanavyokufa wanadamu, na akatuachia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah zake ili ziwe nuru tunayoongozwa kwayo. Kila anayemfanya yeye kuwa mwombezi bila idhini ya Mwenyezi Mungu, au anayedhani kuwa anamiliki wokovu kwa sababu tu ya ukoo au mapenzi, basi amekwenda kinyume na Qur’ani. Hakuna mtu anayemiliki uombezi wala hesabu isipokuwa Mwenyezi Mungu, na hakubaliki yeyote kwake isipokuwa yule aliyekuja na moyo safi.”

Uislamu unaijenga Jamii yenye Huruma
Kuhusu muamala sahihi wa Kiislamu na wengine, Al-Shurafaa Al-Hammadi anasema: “Uislamu haujui ugaidi, na hautoi udhuru wa kuua, kutisha au kudhulumu, bali ni wito wa elimu, kusaidia wengine, na kujenga jamii juu ya msingi wa rehema. Mwenyezi Mungu ametuamuru kujirekebisha wenyewe kabla ya kuwalingania wengine, na kueneza neno zuri na si fitina, kwa sababu fitina inaua amani kutoka kwenye mizizi yake. Siku ya Kiyama, watu watasimama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya hesabu, na hakuna kitakachowaombea isipokuwa matendo mema na imani. Aliyemwamini na kufanya heri ataingia Peponi, na aliyekufuru na kuendelea katika dhuluma yake, basi mafikio yake ni Jahannam, na ni mahali pabaya mno pa kurejea. Uislamu hauuzi Pepo kwa mtu yeyote, na hauitoi kama zawadi kwa kundi fulani, bali ni ya yule anayeistahili kwa imani na ucha Mungu wake.”

 

Uislamu ni Dini ya Amani isiyojua Uadui
Al-Shurafaa Al-Hammadi anahitimisha maelezo yake katika mada hii kwa kusema: “Mwisho kabisa, vita katika Uislamu havipiganwi kwa ajili ya uvamizi, bali kwa ajili ya kujilinda na kulinda wanaodhulumiwa. Na adui akichagua amani, basi ni wajibu wetu kuchagua amani. Hata katika mapigano, Uislamu unatuamuru kuwa na huruma; mateka hawafanyiwi vitendo vya kikatili wala kudhalilishwa, bali wanafundishwa na kupewa heshima. Hivyo ndivyo ulivyo Uislamu, ni wito kwa wenye akili, na si silaha mikononi mwa wenye misimamo mikali ya kijinga. Ni njia ya wokovu na si ya fitina, na ni ujumbe kwa walimwengu wote na si kwa kikundi kimoja pekee. Yeyote anayetaka amani na kutafuta haki, basi atapata katika Uislamu njia ambayo nuru yake haizimiki na kiini chake hakibadiliki. Ni dini ya akili, uadilifu, na rehema, si wito wa chuki au tamaa ya dunia, bali ni mwito kwa moyo wa dhati unaomtafuta Mwenyezi Mungu kiukweli.”

 

موضوعات ذات صلة

زر الذهاب إلى الأعلى